Jokate Mwegelo, Dk. Criss Mauki wametangazwa kuwa washehereheshaji
katika maadhimisho ya Siku Ya Msanii Tanzania yanayotarajiwa kufanyika
Oktoba 25 mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City.
Akizungumza jijini
Dar es Salaam, Mratibu wa Siku Ya Msanii, Justin Jones alisema kutakuwa
na washehereheshaji watatu katika siku hiyo ambapo Criss, Jokate
wataungana na MC mwingine Siza Daniel katika kupendezesha shughuli
hiyo.
“Tulikuwa na idadi kubwa ya watu ambao walitajwa ili wawe Ma-MC
katika shughuli yetu lakini baada ya kutafakari tukabaki na majina haya
matatu ambao wanaingia kwenye historia ya kuwa washehereshaji wa kwanza
katika Siku hii ya kwao,” alisema.
Akizungumzia taarifa ya kuchaguliwa
kwake kuwa MC wa Siku Ya Msanii, Dk. Mauki alisema alifurahishwa na
uamuzi huo kwa kuwa ni tukio kubwa ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza
nchini.
“Nilifurahi sana, kwangu si mara ya kwanza kufanya kazi na
Haak Neel Production, lakini kwa hili Tamasha ni la kitaifa na
linafanyika kwa mara ya kwanza, kwangu ni furaha kuhusishwa nalo, ni
heshima kwangu, ingawa nimeshafanya shughuli kwenye majukwaa mengine
lakini hili litaniongezea heshima, zaidi,” alisema.
Dk. Mauki ni
mwanasaikolojia ambaye amekuwa akitoa mafunzo mbalimbali kupitia
vipindi mbalimbali vya radio, televisheni mijadala na kwenye magazeti.
Jokate amekuwa akifanya shughuli za ushehereshaji katika shughuli
mbalimbali ambapo pia ni mtangazaji wa kituo cha Televisheni cha TV1 cha
mjini Dar es Salaam akiwa na pia anafanya kazi na DSTV ya Afrika
Kusini. Ni mrembo ambaye aliweza kufanya vizuri alipokuwa Balozi wa
kinywaji cha Redds mwaka 2006, ambapo ilidhaniwa kuwa ndiye angekuwa
Miss Tanzania lakini alikuwa Miss Photogenic katika mashindano ya Miss
Tanzania mwaka huo.
Kwa upande wake Siza, alikuwa mtangazaji wa kituo
cha Clouds FM, na baadae kuwa MC katika shindano la Bongo Star Search
pamoja Dume Challenge.
Siku Ya Msanii Tanzania inaandaliwa na Kampuni
ya Haak Neel Production kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa
(BASATA) ambapo imedhaminiwa na New Habari (2006) LTD kupitia magazeti
ya Dimba, Bingwa, Mtanzania na The African, Channel Ten, Magic FM,
Michuzi Media, PSPF, Proin Tanzania, Azam Media na CXC.
No comments:
Post a Comment