Msanii mkongwe na gwiji wa muziki
wa taarabu na ngoma za unyago nchini, Fatma binti Baraka ‘Bi
Kidude (113)’, amefariki dunia huko Bububu, nje
kidogo ya mji wa Unguja na anazikwa leo.Hakika Tanzania nzima na Afrika imepatwa na Simanzi kubwa kuondokewa na Msanii mahiri wa aina yake
Kwa mujibu wa habari za ndugu na jamaa wa marehemu, Bibi Kidude alifariki dunia jana baada ya kuugua maradhi mbali mbali na umri mkubwa.
Mjukuu wake wa kulea, Omar Ameir, alisema mipango ya mazishi inafanywa na anatarajiwa kuzikwa leo saa 7 mchana kijijini kwao Kitumba katika wilaya ya Kati mkoa wa Kusini Unguja.
“Bi Kidude alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya miguu na tumbo kutokana na uzee kwa zaidi ya miezi sita sasa,” alisema mjukuu wake aliyejitambulisha kwa jina la Fatuma.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Pandu Ameir Kificho, alisitisha shughuli za Baraza la Wawakilishi kwa dakika mbili, na kutangazia wajumbe kuhusu taarifa za kifo cha msanii huyo.
“Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, nasikitika nimepata taarifa za kifo cha Bibi Kidude kutoka kwa ndugu na jamaa zake hivi sasa...tumwombee marehemu Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” alisema.
Rais Jakaya Kikwete alimtumia salamu za rambirambi Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara, kutokana na msiba huo.
“Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha msanii mkongwe na mwimbaji mashuhuri wa nyimbo za mwambao nchini, Bibi Fatma binti Baraka,” alisema Rais Kikwete katika salamu hizo.
Aliongeza kuwa alimfahamu Bibi Kidude enzi za uhai wake, kutokana na mchango wake mkubwa ndani na nje ya nchi, katika nyanja za sanaa na utamaduni.
Alimsifu kwa kumudu kuitangaza vema nchi, kupitia kipaji chake cha uimbaji kwenye matamasha aliyowahi kuhudhuria, na uimbaji wake kuwa kivutio kikubwa kwa wengi waliohudhuria matamasha hayo, kuyasikiliza kwenye redio na kuyatazama kupitia matangazo ya televisheni.
“Kwa hakika fani ya sanaa na utamaduni imepoteza mtu muhimu, ambaye mchango wake ulikuwa bado unahitajika katika kuinua kiwango cha uimbaji wa muziki wa mwambao, ambao umejizolea sifa nyingi,” alisema Rais Kikwete katika salamu hizo.
Mara baada ya taarifa za msiba huo, watu wakiwamo wasanii, waandishi wa habari na wapiga picha, walikusanyika nyumbani kwake Rahaleo kutoa salamu za pole na kupata taarifa za kina.
Bi Kidude ambaye alionekana hadharani mara ya mwisho wakati wa Tamasha la Sauti za Busara, kifo chake kimeacha pengo kubwa katika sanaa ya taarab na ufundaji wa unyago.
Bi Kidude alipata kuolewa mara mbili, lakini hakubahatika kupata mtoto.
Kutokana na mchango wake katika sanaa, utamaduni na muziki, alitunukiwa Nishani ya Uhuru mwaka 2012.
Bi Kidude aliyezaliwa kijiji cha Mfagimarigo Zanzibar, anatoka familia ya watoto saba. Baba yake Mzee Baraka, alikuwa mfanyabiashara wa nazi.
Yeye alipata kusema hajui hata tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa alijua alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na kabla ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia.
Bi Kidude alianza kuimba akiwa na umri wa miaka 10 na akijifunza kwa Msanii mkongwe Sitti binti Saad.
Alipata kukaririwa akisema alipotimiza miaka 13, alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania Bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa, aliolewa ingawa ndoa hiyo haikudumu kutokana na manyanyaso ya mumewe.
Kwa hali hiyo, alikimbilia Kaskazini mwa Misri katika miaka ya 1930, ambako aling'ara katika fani ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini katika miaka ya 1940 alirudi Zanzibar na kuendelea na uimbaji.
Katika uhai wake alifanya pia biashara ya wanja na hina, huku pia akijishughulisha na tiba ya mitishamba na unyakanga.
Alitembelea nchi nyingi ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Finland, Ujerumani na Uingereza, sambamba na hilo alipata tuzo ikiwa ni pamoja na ya Tamasha la Filamu ya Nchi za Majahazi (ZIFF) mwaka 1999 ambayo ni ya maisha; alipata pia Tuzo ya WOMAX.
Moja ya nyimbo alizowahi kuimba ni ule maarufu wa ‘Muhogo wa Jang'ombe’, huku pia akiwa na uwezo wa kuimba kwa Kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Koran.
No comments:
Post a Comment