Friday, October 17, 2014

Mrembo Jokate kusherehesha Siku ya Msanii Duniani!!

Jokate Mwegelo, Dk. Criss Mauki wametangazwa kuwa washehereheshaji katika maadhimisho ya Siku Ya Msanii Tanzania yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu katika ukumbi wa Mlimani City. 

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mratibu wa Siku Ya Msanii, Justin Jones alisema kutakuwa na washehereheshaji watatu katika siku hiyo ambapo Criss, Jokate wataungana na MC mwingine Siza Daniel katika kupendezesha shughuli hiyo.
“Tulikuwa na idadi kubwa ya watu ambao walitajwa ili wawe Ma-MC katika shughuli yetu lakini baada ya kutafakari tukabaki na majina haya matatu ambao wanaingia kwenye historia ya kuwa washehereshaji wa kwanza katika Siku hii ya kwao,” alisema. 
Akizungumzia taarifa ya kuchaguliwa kwake kuwa MC wa Siku Ya Msanii, Dk. Mauki alisema alifurahishwa na uamuzi huo kwa kuwa ni tukio kubwa ambalo linafanyika kwa mara ya kwanza nchini.  
“Nilifurahi sana, kwangu si mara ya kwanza kufanya kazi na Haak Neel Production, lakini kwa hili Tamasha ni la kitaifa na linafanyika kwa mara ya kwanza, kwangu ni furaha kuhusishwa nalo, ni heshima kwangu, ingawa nimeshafanya shughuli kwenye majukwaa mengine lakini hili litaniongezea heshima, zaidi,” alisema. 
 

Dk. Mauki ni mwanasaikolojia ambaye amekuwa akitoa mafunzo mbalimbali kupitia vipindi mbalimbali vya radio, televisheni mijadala na kwenye magazeti. 
Jokate amekuwa akifanya shughuli za ushehereshaji katika shughuli mbalimbali ambapo pia ni mtangazaji wa kituo cha Televisheni cha TV1 cha mjini Dar es Salaam  akiwa na pia anafanya kazi na DSTV ya Afrika Kusini.  Ni mrembo ambaye aliweza kufanya vizuri alipokuwa Balozi wa kinywaji cha Redds mwaka 2006, ambapo ilidhaniwa kuwa ndiye angekuwa Miss Tanzania lakini alikuwa Miss Photogenic katika mashindano ya Miss Tanzania mwaka huo.  
Kwa upande wake Siza, alikuwa mtangazaji wa kituo cha Clouds FM, na baadae kuwa MC katika shindano la Bongo Star Search pamoja Dume Challenge.  

Siku Ya Msanii Tanzania inaandaliwa na Kampuni ya Haak Neel Production kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambapo imedhaminiwa na New Habari (2006) LTD kupitia magazeti ya Dimba, Bingwa, Mtanzania na The African, Channel Ten, Magic FM, Michuzi Media, PSPF, Proin Tanzania, Azam Media na CXC.

No comments:

Post a Comment