Wednesday, October 21, 2009

Waliotengeneza "koNyagi" bandia wahukumiwa..!!!

MAHAKAMA ya Wilaya ya Temeke imewahukumu kwenda jela miaka mitano au kulipa faini ya sh. 300,000 kila mmoja washitakiwa watatu baada ya kuwatia hatiani kwa makosa matatu likiwemo la kutengeneza pombe haramu kwa kutumia nembo ya Konyagi.

Katika hukumu yake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Temeke, Bi. Hellen Riwa alisema mahakama imeridhika kuwa washtakiwa hao wamepatikana na hatia ya kutenda makosa matatu.

Alisema washtakiwa hao Beda Mavinga, Mohamed Rashid na Aden Karim wamekutwa na makosa ya kutengeneza pombe ya konyagi bandia, kutumia nembo ya konyagi kwa nia ya kuziuza na kupatikana na mali ya wizi kinyume cha sheria.

Hakimu Riwa alisema kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka uliongozwa na Mrakibu wa Polisi, Bw. Basil Pandisha washtakiwa hao walihusika katika kosa hilo, hivyo wanastahili adhabu kali.
Alisema kutokana na makosa hayo aliwahukumu kwenda jela miaka 5 au kulipa faini ya sh. 300,000 kila mmoja.

Washtakiwa hao walikamatwa na Jeshi la Polisi Septemba 7, mwaka jana katika eneo la Makangarawe, Temeke wakitengeneza pombe na kuweka nembo ya Konyagi na nembo ya Mamlaka ya Kodi ya Mapato Tanzania (TRA) kwa nia ya kuziuza.

Washtakiwa hao kwa pamoja walilipa faini ya sh. 300,000 kila mmoja na kuachiwa huru. Ameripoti Peter Mwenda www.majira.co.tz

No comments:

Post a Comment