World News

Tuesday, November 11, 2014

Mrejesho wa kikao na Prof. Tibaijuka juu ya Mji mpya wa Kigamboni!!

FAUSTINE NDUGULILE,Mbunge wa Kigamboni
Siku ya Jumapili tarehe 10 Agosti 2014 kilifanyika kikao cha mashauriano kuhusu Mpango Kabambe wa Uendelezaji Mji Mpya wa Kigamboni kilichojumuisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Prof. Anna Tibaijuka (Mb), Waheshimiwa Madiwani, Maofisa Watendaji Kata, Mbunge wa Kigamboni na wadau wengine. Mhe. Waziri alielezea kuwa lengo la kikao hiki ni pamoja na kutoa elimu kuhusu suala la hisa na kutaka kuwashawishi Madiwani na Mbunge kulikubali suala hili na pia kutoa taarifa ya vikao vya “Public Hearing” alivyotaka kuanza kuvifanya kwenye kata mbali mbali za Jimbo la Kigamboni kuanzia tarehe 24-29 Agosti, 2014.

Proj. Anna Tibaijuka


MAELEZO YA MHESHIMIWA WAZIRI 

Mhe. Waziri alitumia muda mwingi “kutoa darasa” kuhusu suala la hisa, umuhimu wake na jinsi wananchi wa Kigamboni “watakavyobaki kwenye ardhi yao kupitia hisa”. 

MAMBO YALIYOJITOKEZA KATIKA MJADALA HUO 

Washiriki wa kikao walionyesha kutoridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Mji Mpya wa Kigamboni. Washiriki wa kikao walimweleza Mhe. Waziri kuwa wananchi wa Kigamboni wanataabika kwa muda wa miaka sita sasa. Wananchi hawajengi, hawakarabati, hawauzi na wala hawakopesheki. Vile vile washiriki walionyesha wasi wasi kuhusu suala la hisa na kutaka hisa iwe ni hiari. Washiriki wa kikao walimtahadharisha Mhe. Waziri kuhusu kufanya mikutano kwenye kata nyingine za Jimbo la Kigamboni kabla ya kutatua matatizo 
ya Uvumba na Kifurukwe katika Kata ya Kibada kwanza. Vile vile walitaka kujua kama fedha ya kulipa fidia ipo kwa wananchi wa Uvumba na Kifurukwe ziko tayari. Mimi kama Mbunge, nilihoji uhalali wa suala la hisa kwa kuuliza maswali yafuatayo: 

1. Ni sheria ipi inayotumika kufanya suala la hisa kuwa ni lazima kwa wananchi wa Kigamboni? 

2.Ni lini wananchi waliridhia kukatwa asilimia 10 ya fedha zao za fidia kwa ajili ya hisa? Kwa nini isiwe pungufu au zaidi ya kiwango hiki? 
3.Hizo fedha watakazokatwa toka kwa wananchi zitaenda wapi?

4. Chombo cha kusimamia hisa hizo kilianzishwa lini na kwa sheria ipi? 

5. Usimamizi wa chombo hicho ukoje? 

6. Fedha hizi zitatumikaje?

7.Masuala ya gawio yatakuwaje? Vile vile, niliunga mkono mawazo ya Washiriki wa kikao kuwa Wizara ijikite zaidi kwenye eneo la Kifurukwe na Uvumba kabla ya kwenda maeneo mengine.

Aidha, nilimkumbusha Mhe. Waziri kuhusu kutekeleza maagizo mbalimbali kama yafuatayo: 
1. Kurudisha mrejesho kwa Baraza la madiwani la manispaa ya Temeke juu ya hoja walizozitoa katika kikao chao cha mwisho na Mhe. Waziri

. Jambo hili halijatekelezwa hadi hivi sasa. 

2.Maagizo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira kupitia kwenye hotuba yake katika mkutano wa 15, kikao cha 20 cha Bunge kilichofanyika tarehe 28 Mei 2014. Kamati ya Bunge ilitoa maagizo kwa Wizara na kutaka maelezo ya utekelezaji ya maagizo hayo kuwasilishwa kwenye Kamati hiyo. Maagizo haya hayajafanyiwa kazi. 

3. Mheshimiwa Waziri Mkuu wakati anahitimisha bajeti ya Wizara yako alisema yafuatayo:“Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niseme tu kwamba, niliposikiliza taarifa ya kamati na kama mtaona Taarifa ya Kamati na kama mtaona ukurasa wa 22 na 23 na zile kurasa za mwisho kwenye hitimisho, yapo mawazo ambayo nafikiri ni mazuri sana. Kinacholeta tatizo hapa inaonekana pengine Serikali hatujafanya kazi ya kutosha katika kuelimisha jamii juu ya mradi wenyewe, namna utakavyosimamiwa, utakavyoendeshwa na kubwa zaidi dhana hizi mpya za hisa, unajua ni dhana ambazo zinahitaji elimu ya kutosha. Hata haya mambo mengine ambayo yanadaiwa hapa ya kutoshirikishwa na kadhalika, kwa sababu yamesemwa hapa ndani ya Bunge, mimi nadhani jibu sahihi tukubali

Tukubaliane na aliyosema Mheshimiwa Ndugulile pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine kwamba, acha Serikali jambo hili tulichukue upya, tupitie maeneo yote ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyasema, tutashirikisha Wabunge wenyewe na zile Wizara zote ambazo zinahusika,
Kubwa ni Baraza la Madiwani katika Manispaa ya Temeke, maana eneo hili mpende msipende, ni eneo ambalo lipo chini ya Manispaa hiyo. Tulichofanya ni kuchukua eneo kwa madhumuni ya uendelezaji, lakini hatuwezi kuacha lile Baraza bila kulielimisha kiasi cha Kutosha (Makofi). Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka nikuhakikishie, na niwaombe wenzangu kwamba, Serikali acha ilipe uzito unaotakiwa, naamini tutafikia mahali pazuri tu bila tatizo kubwa (Makofi)"

Nilimhoji Mhe. Waziri kuhusu utekelezaji wa mapendekezo ya Kamati ya Bunge na maagizo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu yamefikia wapi? Ni lini yatatekelezwa? Kwani kuendelea hatua nyingine za utekelezaji wa Mradi pasipo kutekeleza maagizo ya Kamati ya Bunge na Waziri ni kuonyesha dharau kwa mamlaka ya Taasisi ya Bunge na Ofisi ya Waziri Mkuu. 

MAJIBU YA WAZIRI 

1.Mhe. Waziri alikubali kuwa suala la hisa litakuwa ni hiari. Alikiri kuwa hadi sasa hakuna chombo cha kusimamia hisa za wananchi na kwamba suala hili litajulikana baada ya wataalam washauri wa Wizara wakakapomaliza kazi ya kuandaa prospectus”. 

2. Mhe. Waziri alikubali kusitisha mikutano kwenye kata nyingine na kujikita zaidi kwenye mitaa ya Uvumba na Kifurukwe.

3. Waziri alikiri kuwa kwa sasa hana fedha ya kutosha kuwalipa wananchi wote waliokubali kufanya uthamini kwenye mitaa ya Kifurukwe na Uvumba. Ikumbukwe kiasi cha Tsh 32 Billioni kinahitajika kulipa wananchi 228 ambao ni sehemu ya wananchi zaidi 2000 waliokubali kufanya tathmini. Wizara hadi sasa ina kiasi cha Billioni 9 tu.

MAKUBALIANO 

1. Suala la hisa liwe ni la hiari. Wananchi waelimishwe na waamue kujiunga kwenye mfumo wa hisa kwa hiari yao. Kusiwepo na masharti ya kulazimisha ukataji wa hisa kabla ya kupokea fidia. 

2. Mikutano ya Public Hearing isitishwe na badala yake nguvu za Wizara zielekezwe kwenye eneo la Uvumba na Kifurukwe ili mafanikio ya maeneo haya yatoe hamasa kwa wananchi wa Kata nyingine. 

3. Utelekezaji wa maazimio haya uende sambamba na utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya Bunge na maagizo ya Waziri Mkuu. 

HITIMISHO 

Nawaomba wananchi wa Kigamboni, hususan Uvumba na Kifurukwe kuendelea kuwa wavumilivu wakati tunaendelea kufanyia kazi makubaliano haya na maagizo mengine yaliyowahi kutolewa na vyombo vingine ambayo hayajatekelezwa na Wizara hadi hivi sasa. 


Dkt Faustine Ndugulile (MB)

JIMBO LA KIGAMBO

No comments:

Post a Comment

Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...
Related Posts Plugin for WordPress, Blogger...