Msanii wa muziki wa Hip Hop nchini anayetamba na single zake za 'Choo cha Kike', Hiphop imenoga, Kindumbwendubwe na ngoma yake mpya ya Skiliza Mchumba, Omary Muba a.k.a 'Ommy G' amelalamikia ubovu wa Kampuni ya upato ya Development Enterprenueship Community Initiative (DECI) kutowalipa wateja wake kitu kinachowakwamisha kufanya mambo mbalimbali waliyopanga katika maisha yao.
Ommy G (pichani) alisema kuwa yeye alipanda mbegu zake tangu mwezi Aprili mwaka huu na kutegemea kuvuna Juni mwaka huu, ambapo ameshindwa kuvuna mbegu zake baada ya DECI kufungiwa kuendesha biashara zake wanazozifanya kinyume na sheria.
Alisema kuwa kufuatia kutovuna mbegu hizo kutoka katika Kapuni ya DECI, kumemfanya kushindwa kuendeleza ndoto zake alizokuwa amepanga kufanya katika matarajio ya kuendeleza maisha yake kwa mwaka huu.
Alisema kuwa kitendo hicho kinazidi kumkosesha amani kila siku zinavyozidi kwenda ambapo anakosa matumaini ya kuzipata na kufanya ndozo zake kuendelea kufififia kila siku.
Alisema kuwa alikuwa ana mpango endelevu na matumaini kuwa baada ya kuvuna mbegu zake, aende kusomea kozi ya Uandishi wa Habari pamoja na kuiingiza albam yake sokoni ambayo tayari imekamilika ikiwa na jumla ya nyimbo 10 alizorekodia kwenye studio mbalimbali.
Ommy G alisema kuwa albam hiyo ina nyimbo 10 ambazo ameshirikisha wasanii mbalimbali ikiwa ni pamoja chipukizi kwa ajili ya kutoa ujumbe na kuburudisha jamii na mashabiki wake ambapo kwa sasa anatarajia kuitambulisha rasmi Agosti 8 mwaka huu.
"Baada ya kupanda mbegu zangu DECI, sikujua kuwa kampuni hiyo haijasajiliwa mi nilijua ni ya halali ambapo nilitarajia kuvuna mbegu zangu mwezi huu, kwa ajili ya kufanya mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kujiendeleza kimasomo lakini ndoto zangu zinazidi kufifia kutokana na DECI kufungiwa, na itakuwa imetuangamiza sisi watu wa hali ya chini ambao hatuna kazi" alisema Ommy G.
Ommy G alizitaja baadhi ya nyimbo zake kuwa ni pamoja na Choo Cha kike aliyomshirikisha D. Knob, Sikiliza Mchumba aliyofanya na Dulayo, Kindumbwe ndumbwe, Rudi mwana , Nakupenda na Muumba.
Mgogoro wa DECI ulianza baada ya Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania kutoa onyo kwa wananchi waliokuwa wakiweka fedha zao ambapo iliwataka kuacha kwa kuwa ilikuwa haijasajiliwa na kufuata taratibu za fedha.Mpaka sasa wanachama wa DECI hawajui hatma ya kupata fedha zao ambazo walizipanda kama mbegu kwa matumaini ya kuvuna zaidi ambapo baadhi ya viongozi wa DECI wanaoshitakiwa kwa sakata hilo ni Bw. Jackson Mtares, Bw. Dominick Kigendi, Bw. Timotheo Ole Loitg'nye, BW. Swamel Mtares na Bw. Arbogast Kipilimba wote wakazi wa Dar es Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment